TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KUJIUNGA NA KIDATO CHA TANO, VYUO VYA UALIMU NA VYUO VYA ELIMU YA UFUNDI MWAKA, 2020
Jumla ya wanafunzi 121,251 wakiwemo wasichana 53,829 na wavulana 67,422 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano, Vyuo vya Ualimu, na Vyuo vya Elimu ya Ufundi vinavyosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE). Idadi hii ni sawa na asilimia 93.4% ya wanafunzi wenye sifa za kuchaguliwa.Wanafunzi wa Kidato cha Tano:
Wanafunzi wote wa bweni waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano mwaka 2020 wanatakiwa kuripoti shuleni tarehe 18 Julai, 2020 tayari kwa kuanza masomo tarehe 20 Julai 2020.Aidha, wanafunzi wa kutwa waripoti na kuanza masomo tarehe 20 Julai 2020. Wanafunzi ambao hawataripoti wiki mbili tangu tarehe ya kufungua shule nafasi zao zitachukuliwa na wanafunzi wengine ambao hawakupangiwa shule katika awamu hii.
Uhamisho wa shule utaruhusiwa baada ya kukamilika kwa Muhula wa Kwanza wa masomo, na zoezi hilo litafanyika kwa kuzingatia uwepo wa nafasi kwenye Shule kwa idhini ya Maafisa Elimu wa Mikoa husika. Hivyo, hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya Shule kwa sasa ngazi za Mikoa Halmashauri na shule.
Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Ufundi:
Wanafunzi waliopangwa kwenye Vyuo vya Elimu ya Ufundi vilivyopo chini ya NACTE wanatakiwa:๐ Kuthibitisha kukubali kujiunga na kozi zinazosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) baada ya siku saba (7) kuanzia siku ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi hadi tarehe 15 Agosti, 2020.
๐ Mwanafunzi atafanya uthibitisho kupitia kiunganishi kinachoitwa Uthibitisho TAMISEMI katika tovuti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ambayo ni www.nacte.go.tz ili kukubali kuchaguliwa kwenye kozi na vyuo walivyopangiwa.
๐ Mwanafunzi ambaye hatathibitisha kukubali nafasi aliyochaguliwa, nafasi yake itachukuliwa na wanafunzi wengine wanaoendelea kuomba katika Vyuo hivyo kwa njia ya mtandao.
๐ Wanafunzi wanaotaka kufanya mabadiliko ya kozi au chuo walikochaguliwa, wanaruhusiwa kufanya hivyo kuanzia tarehe 01 Agosti hadi 30 Agosti, 2020 kupitia mtandao wa NACTE.
๐ Vyuo ambavyo vimepangiwa wanafunzi, vitapata orodha ya waliochaguliwa kutoka NACTE kwa njia ya Mfumo (kupitia Institution Pannel) baada ya muda wa kuthibitisha na kuhama kukamilika.
๐ Maelekezo ya namna ya kuwasajili wanafunzi watakaoripoti Vyuoni kuanza masomo yatatolewa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
๐ Wanafunzi waliopangwa katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya hawatahusika na utaratibu wa kubadilisha wa NACTE, hivyo wanapaswa kuwasiliana na vyuo husika.
Source: https://www.tamisemi.go.tz/announcement/taarifa-kwa-umma-kwa-wanafunzi-waliochaguliwa-kujiunga-kidato-cha-tano-na-vyuo-vya-kati
Imetolewa na: Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - TAMISEMI.
===============================